Babati.Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amewataka wawekezaji wa ndani kutumia fursa ya uhitaji wa pembejeo kuongeza uzalishaji.
Amesema kwa sasa Serikali inaagiza takribani tani 700,000 za mbolea nje ya nchi.
Alieleza hayo jana Jumamosi Aprili 17, 2021 alipofanya ziara katika kiwanda cha mbolea cha Minjingu kilichopo Wilaya ya Babati kuangalia shughuli za uzalishaji zinazoendelea katika kiwanda hicho.
"Sasa hivi tunataka pembejeo zipatikane kwa wakulima kwa gharama nafuu na kwa wakati, mahitaji yetu ya pembejeo tutumie kama fursa ya kuongeza uzalishaji ndani ya nchi yetu."
"Tuongeze kasi ya uzalishaji ili hii mbolea ambayo tunaagiza nje iweze kuzalishwa hapa Minjingu, tunataka vya kwetu kwanza ili mradi vinakuwa na viwango vinavyotakiwa na kwa bei nafuu ambayo mkulima anaweza kumudu," amesema Profesa Mkenda.
Amewaalika wawekezaji wanaotaka kuja nchi kuwekeza kwenye pembejeo na kwamba Serikali itasimama nao na kuwapa upendeleo.
"Tunawaalika wawekezaji popote walipo waje wazalishe mbolea hapa nchini, hatutajali uraia wake tutampa upendeleo maalumu ,tutawalinda na tutasimama nao,"amesema Profesa Mkenda.
Post a Comment