KIKOSI cha Simba tayari kipo mjini Shinyanga kwa ajili ya mchezo wao wa leo jioni wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao, Mwadui, lakini unaambiwa nyota wa kigeni wa timu huyo wakiongozwa na Meddie Kagere, Clatous Chama na Luis Miquissone balaa lao katika VPL si mchezo.
Nyota hao wa kigeni ndio wanaoonekana kuibeba timu hiyo si tu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pekee lakini zaidi ni katika Ligi Kuu msimu huu na kuiweka pazuri timu yao kutetea ubingwa wake.
Simba ilirejea Ligi Kuu majuzi kwa kishindo ikiifumua Mtibwa Sugar mabao 5-0 huku mabao yote katika mchezo huo yakifungwa na mastaa wa kigeni na kupunguza pengo la pointi baina yao na vinara Yanga kuwa mbili tu.
Kama hujui tu ni kwamba Simba ndio timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi ikiwa imefunga mabao 51 ikifuatiwa na Yanga iliyofunga mabao 37.
Kati ya mabao hayo 51 ambayo Simba imefunga 33 yamefungwa na mapro wa kigeni huku 18 tu yakifungwa na wazawa wakiongozwa na nahodha John Bocco mwenye mabao tisa.
Mnyarandwa Meddie Kagere ndiye anayewapaisha wageni akifunga 11 na kuwa kinara wa orodha ya wafungaji wa ligi hiyo, huku akiongoza pia ndani ya Simba, akifuatiwa kwa mbali na Chama aliyefunga mabao saba akifuatiwa na Luis Miquissone wa Msumbiji aliyefunga mabao matano sawa na mcongo Chriss Mugalu.
Mghana Benard Morrison yeye amefunga mabao matatu, akifuatiwa na mzambia Rarry Bwalya, muivorycoast Pascal Wawa na mkenya Joash Onyango waliofunga bao moja kila mmoja.
Staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel alisema; “Hili ni tatizo tena ni kubwa, ninachoshauri watengenezwe wengine wawe wanawapa nafasi mara moja moja kama Miraji Athuman ambaye huwa anaonyesha kiwango kizuri akicheza, lakini akiwa anategemewa Bocco akiumia anakosekana mshindani inakuwa changamoto.”
“Tafsiri yake ni kwamba Simba, Yanga na Azam wafungaji wakiwa ni wageni tu vipi kuhusu timu yetu ya Taifa Stars, itakuwa na washambuliaji wa aina gani, hili ni jambo lakuchukuliwa kwa uzito kuwaandaa wafungaji wazawa kwenye timu zetu ambao watakuwa wanashindana na hao kina Kagere wakiwa kwenye timu zao za taifa,” alisema.
Nyota wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala alisema; “Simaanishi kwamba ni kitu kibaya wageni kupambana kuonyesha uwezo wao kwani ni kazi iliyowaleta Tanzania.
“Ila wazawa wanapaswa kujituma wakitambua kwamba kuna timu ya taifa ambapo mara nyingi wanakuwa wanakutana na timu zao hao wanaocheza nao na kujikuta wanapata wakati mgumu wa kupata matokeo, hili lazima waliangalie kwa umakini,” alisema. Mastaa wa Simba wamekuwa na kasi ya mafanikio ambayo imezidisha chachu kwenye mbio za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Post a Comment